Monday, November 17, 2008

Tip Top wazamisha wawili Kisima Awards



Wasanii kutoka familia ya Tip Top Organization, Cassim na Z-Anto wametajwa kuwania tuzo maarufu zinazotolewa nchini Kenya, ‘Kisima Award’ kwa mwaka 2008/2009.

Tuzo hizo zimepangwa kufanyika Novemba 29 mwaka huu, ambako Cassim anayetamba hivi sasa na vibao vyake vya ‘Awena’ na ‘Sababu’, ametajwa kuwania kipengele cha wimbo bora wa mwaka kwa upande wa Tanzania, kupitia kibao chake cha ‘Haiwezekani’.

Wasanii wengine anaokabiliana nao na nyimbo zao kwenye mabano ni pamoja na Ali Kiba (Mac Muga), Matonya (Haiwezekani), Nakaaya Sumari (Mr. Politician), na TMK Wanaume Family (Dar Mpaka Moro).

Kwa upande wake, Z-Anto anayetamba na wimbo wake wa ‘Binti kiziwi’, ametajwa kupitia kibao hicho, kuwania tuzo ya video bora ya mwaka, ambako kipengele hicho kinawaniwa pia na TID (Nyota Yako), AY na Mwana FA (Nangoja Ageuke), Lady Jaydee (Siku Hazigandi) na Marlaw (Bembeleza).

Pia msanii Matonya, ametajwa kuwania tuzo ya wimbo bora wa ushirikiano, ambako wimbo wake wa ‘Anitha’ aliomshirikisha Lady Jaydee utawania pamoja na zile za ‘Una’ wa P Unit na DNA, ‘Mbali nami’ wa Juliana na Bushoke, ‘Kumekucha’ wa Nonini, Q Chillah na Prof Jay.

Matonya pia anawania tuzo ya mwanamuziki bora wa kiume wa Afrika Mashariki, akiwa na Mejja, Nameless, Navio na Onyo Papa J, huku kwa upande wa wanawake, Lady Jaydee atachuana na Juliana Kanyomozi, Marion Shako, Nyota Ndogo na Stl.

Kadhalika, kundi la Wanaume TMK limeteuliwa kuwania kundi bora la Afrika Mashariki, sambamba na kundi la Klear Kut, P Unit, Ukoo Fulani na Wakenya Pamoja.

No comments: